MCHUNGAJI HARUHUSIWI KUGOMBEA UONGOZI WA KISIASA SERIKALINI

Nakusalimu rafiki na ndugu yangu katika kristo Yesu. Bwana asifiwe!

Tufurahi katika Bwana tukijua majina Yetu yameandikwa katika kitabu cha mbinguni; sio vinginevyo! Tusifurahi kwa sababu sisi tunasifiwa makanisani kuwa watoaji wazuri ama waimbaji wazuri ama walimu wazuri ama wenye upako. Yote hayo hata anayekwenda motoni huyapata tena na zaidi.

Lipo jambo katika siku hizi za mwisho kwamba mtu kuwa mhudumu yaani kuwa na huduma inamfanya kujiona wa kipekee. Tena Mungu pale anapomtumia kwa viwango katika karama aliyowekewa hutaka kana kwamba Dunia yote imtambue na ajulikane pote; Sio Mungu ajulikane bali yeye ajulikane!

Kuna machaguo mawili tu tuliyopewa yaani Mungu ama shetani. Badala ya Baraka ni laana.
Sasa, KUNA IMANI KUU MBILI DUNIANI; yaani kumwabudu Mungu wa kweli na nyingine ni kinyume cha hiyo.
Kumwabudu Mungu asiye wa kweli inajumuisha WAPAGANI NA VUGUVUGU. Yesu ndiye Mungu hivyo anayeabudu nje ya Yesu huyo ni mpagani pia. Maana roho ya mwanadamu imeumbiwa ibada ndani, hivyo hakuna asiyeabudu.

SIASA Ni moja ya pepo nne za Dunia anazozitumia shetani kujenga ngome zake hapa duniani. SIASA imekuwa ngome imara kwa shetani, hapa ndipo amefanikiwa kwa asilimia mia kukalia kiti na kuuza sera zake. Amedhibiti eneo hili kwa Kuweka sheria serikali kutokuwa na dini; yaani sheria za Mungu hapa zimetupiliwa mbali, akaweka za kwake kama HAKI ZA BINADAMU ambazo nyingine zinapinga moja kwa moja sheria za Mungu. Mfano Ndoa za jinsia moja ni machukizo mbele za Mungu lakini haki za binadamu anasema kila mtu anahaki ya kuchagua; Kuoa ama kuolewa na jinsia tofauti ama jinsia moja. Haki za binadamu anasema ni haki yako kuabudu chochote.

Sasa leo mchungaji anataka kuwa kiongozi katika serikali na wengine wamefanikiwa mpaka kuwa maraisi wa nchi kama Rais wa malawi. Najiuliza swali dogo; kwa nini Mungu hakumweka samweli kuwa mfalme? Alimjua atakuwa mkamilifu mbele zake, badala yake anamtuma samweli kwenda kumpaka mafta Sauli ambaye baadae alikengeuka.

Kwa nini hakumweka mtu kama Eliya, Elisha,Isaya, Yeremia n.k kuwa wafalme maana watu wake wangetenda yaliyo mema juu ya manabii hawa! Unaweza kujiuliza maswali kama hayo? Leo hii Mchungaji/Muonaji anataka kuwa mfalme!!! Tunamtumia Daniel kujihalalishia kuwa ni sawa kugombea; Hivi Daniel wakati akiwa serikalini alikuwa wapi?? Maana Daniel alikuwa utumwani; mahali ambako hawakuwa na mfalme wao bali wa Babel. Hawakuwa na utaratibu wao bali wa Babeli. Daniel hakuwa Mchunagaji wala Nabii bali mmoja wa wenye hekima(mtauwa). Alimtumikia Mungu kwa nafasi yake na Mungu akamheshimisha.
Wapo wa kina Daniel leo katika serikali wakitumika kwa uaminifu na uchaji mzuri juu ya Mungu wetu. Hilo ndilo fungu lao kama ilivyokuwa kwa Daniel. Na mchungaji analo fungu lake kwa kulichunga kanisa. Lakini kama mchungaji atataka kumpangia Mungu atumike vipi mbele zake; Huyo anafanana na mfalme Sauli. Sauli akihakikishiwa na Bwana kuwa atawapiga waamaleki na sharti la Mungu lilikuwa asibakize chochote wala kurudi na nyara. Sauli akataka kumpangia Mungu inavyopaswa amtumikie, akazoa nyara zilizonona kwa ajili ya sadaka. Likawa chukizo kwa Bwana, Mungu alisema KUTII NI BORA KULIKO SADAKA.

19 Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?
1 Samweli 15:19

20 Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
1 Samweli 15:20

21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
1 Samweli 15:21

22 Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
1 Samweli 15:22

23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.
1 Samweli 15:23
Ukiangalia hapo Sauli alikuwa na Lengo zuri tu tena la kumtukuza Mungu, lakini tayari alikuwa ameasi sauti ya Bwana.

Kwa hiyo Wachungaji mnaosema hamna ubaya wowote kugombea Nafasi katika serikali ni kukosa maarifa. Mmewekewa fungu lenu katika hekalu, Na sheria ni ya milele kuwa mtamtumikia Mungu humo(walawi).

Hitimisho
Katika siku za leo; Nabii na makristo wa uongo ndio wamejaa tele. Ni mchungaji wa uongo na nabii/mtume wa uongo ndio anaweza kugombea nafasi serikalini. Usitishwe na Kupokelewa na Watu wengi ukajua Mungu kamwita huku nako awakomboe watu, Hapana! Mungu hajawahi kubadili njia zake. Biblia inasema;
Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.
Luka 6:26
Onyo kali juu ya kusifiwa na watu wote, maana Hata zamani manabii wa uongo walipendwa na kusifiwa na wengi na hata kuwa maarufu katika jamii. Kwa hiyo sifa ya kukubalika na jamii na kuwa maarufu tafsiri yake ni kuwa wewe ni nabii wa Uongo!
Samweli atabaki kuwa nabii na Daudi kuwa mfalme. Mungu anao wa kina Daniel serikalini, usimpangie.

Kinachoshangaza ni watu kuendelea kuwatukuza hawa manabii wa Uongo. Kama waumini wangepata maarifa, hawa manabii na makristo wa uongo wangetoweka kama moshi.

Wafanyao hayo hufanya kwa tamaa zao wenyewe, Mungu wao ni yule ibilisi. Mchungaji kugombea ni dhihirisho la kazi za yule Ibilisi ndani ya huyo mtu aliyokuwa anaifanya katika kanisa, sasa anataka kuipeleka mahali pake sahihi maana huku anaifanya kwa hukumu kubwa ndani yake.

Tokeni kwao enyi watu wa Mungu ili wakati wa mapatilizo msije mkashiriki mapigo yao! Unabii umetimia kuwa na hawa watu. Tokeni kwao.

Shalom!

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

NAO WANIABUDU BURE!

NIMEWAPELEKEA TAUNI KAMA YA MISRI (CORONA) LAKINI HAMKUNIRUDIA MIMI

JE! NAWEZA KUWA SAFI NAMI NINA MIZANI YA UDHALIMU!!