JE! NAWEZA KUWA SAFI NAMI NINA MIZANI YA UDHALIMU!!

Jina la Yesu litukuzwe, Mungu wetu ni Mungu mmoja na jina lake ni Yesu. JINA LAKE LITUKUZWE!!! Karibu tule na kunywa pamoja.

Kwa wapendwa wote katika Kristo na wasio katika kristo, nawasalimu!
Siku hizi ni siku za mwisho, Na ni wakati wa kujitakasa sana na uovu wa dunia hii maana kweli imepotoshwa na watu wakachagua kuuamini uongo na kukataa kweli, Hiyo namaanisha wakristo kuwa vuguvugu, jambo ambalo ni baya kuliko mtu asiyeamini.

Mika 6:11
JE! NAWEZA KUWA SAFI NAMI NINA MIZANI YA UDHALIMU, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu?
Kuna mambo mengi yalikuwa yanaendelea katika Yuda wakati nabii Mika anahubili habari hizi, Yuda ilikuwa imeacha njia ya Bwana na kulinajisi taifa. Wakati huo pia alikuwapo nabii isaya, na mika alihubili na kutabili Yuda kwenda utumwani, Babeli (mika 4:10). Yuda ilionywa kwa mda mrefu kwa kurudi nyuma kwa matendo yasiyo haki, ni kweli walikuwa kanisa la Mungu teule ambao Mungu aliwachagua kwanza kama mzaliwa wa kwanza, wakati huo kanisa lilipoa, wakaanza kuipaka mafuta dhambi ififie. utaona huo msitari juu unawazungumzia kuwa watu wenye kujihesabia haki bure, maana walijihesabia kuwa watakatifu huku matendo yako yakikana huo utakatifu. Hata walipokuwa wanahubiliwa walikuwa wagumu kuelewa maana ni kama dhambi hawakuiona kama ni dhambi, ilimradi mtu anamtolea Bwana sadaka ya nguvu, ilimradi wanafanikiwa katika mashamba basi walijihesabia haki mbele za Mungu. Walitenda dhambi makusudi wakijua watatoa dhabihu/sadaka itakayowasafisha na ni kweli dhabihu ilikuwepo kuwaondolea dhambi, Lakini aliwaambia..

Mika 6:6-8.
6Nikamribie BWANA na kitu gani,na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka ya kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? 7Je! BWANA atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? 8Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda HAKI, NA KUPENDA REHEMA, NA KWENDA KWA UNYENYEKEVU NA MUNGU WAKO!
Pamoja na utoaji mzuri waliokuwa nao, Mungu kwa kinywa cha nabii Mika anawauliza, watamtolea nini kwa ajili kosa lao? kwa lugha nyingine walitenda wakijua ni makosa, jambo ambalo hata ungetoa kitu gani ile dhambi haindoki mpaka umetubu na kuacha mara moja na kwenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu(jinsi anavyotaka Mungu uende) kwa kutenda mapenzi (Haki), na kutaka rehema.

Kama ilivyokuwa kwa Israeli na Yuda, walihubiliwa lakini waliziba masikio. Waliwachukia hata hao manabii wa Mungu, soma kitabu ha Yeremia ambaye aliwaonya Yuda mda mfupi kabla Babeli hawajavamia. Sasa Mika aliwatabilia miaka mingi kabla hata Babeli haijawa na nguvu. Lakini walikaza shingo wakifuata maneno malaini ya manabii wao wa uongo waliokuwa wanawatabilia uongo na kuwatumainisha kuwa wao ni taifa teule, kuna amani, tumefanikiwa mashambani bila shaka wakina Mika ni waongo, wanawaogofya watu bure, tena manabii wa uongo hutumia maandiko haya haya kwa kutumia mifano mizuri kama ile ya wapelelezi 12 wa israeli waliokuwa wameenda kuipeleleza kanaani wakaja na habari mbaya isipokuwa Yoshua na kalebu. Hivyo kweli kila mtu angemwona Mika yu kinyume na neno la Mungu.
Baada ya mda mrefu wakati uliwadia na wakaenda Babeli kama Mika alivyotabili.

Jambo la ajabu tena katika siku hizi dhambi imefifishwa kana kwamba haipo. Wachungaji wamerudi nyuma, Wanakemea kutohudhuria ibada na kutotoa sadaka ila sio kuvaa vimini kanisani ama viduku ama kupaka make-up. Yale mawigi yaliyokemewa sana hapo nyuma wakati yanaanza kuingia kuwa ni kinyume na Neno la Mungu, sasa leo kama mwanamke kanisani havai wigi ni wanne katika kumi na wakati mwingine wawili kati ya hao wanne wamerefusha nywele zao kuwa kama wazungu maana pengine wanadhani Mungu alijisahau kuwaumba wana nywele fupi wakati amesema mwanamke afunikwe na nywele, na waliobaki wawili hawana uwezo wa kugharimikia hayo yote. Kifupi ni kwamba, aliyekoka wa leo hana tofauti na asiyeokaka. kama ni kiduku wote wananyoa, kama ni kufuga kucha ama kupaka rangi wote wanafanya, kama ni kuvaa vimini wote wanavaa isipokuwa baadhi jumapili hawavai, kama ni suruali(wanawake) wote wanavaa, kama ni nguo za kubana wote wanavaa. Kwa hiyo sio chumvi ya ulimwengu tena bali chumvi iliyoharibika na tunajua hamna kitu cha kutia ikakolea.

1Wakorintho 3:16-17.
16hamjui kuwa ninyi mmekuwa Hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? 17kama mtu akiliharibu Hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana Hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Swali dogo ni kuwa unaliharibu vipi hekelu la Mungu(mwili wako)? tumekwisha kuona baadhi ya matendo hayo na yapo mengine kama kuvaa nguo zinazochora maumbile(hili nalo juzi juzi tu lilikuwa linakemewa lakini sasa hivi limepakwa mafta yaani sio dhambi tena kwa wanaomwita Bwana kwa midomo tu), kupaka kucha rangi na kufuga makucha. Hizi tabia mara nyingi Biblia inazitaja kuwa ni za KIKAHABA. na ukweli ni kwamba tabia hizi zote zimetokea hukohuko, Tabia ya Yezebeli ambazo Mungu anazichukia, lakini leo kanisa limelewa chakali na mvinyo wa uashearti huu.
Je! na mimi nimekuwa kama wale 10 walioleta habari mbaya kwa israeli? siku zote wayatendayo mapenzi ya Mungu ni wachache, ndio maana ni Yoshua na Kalebu peke yake walikuwa upande wa Mungu, ni watu wanane tu ndio walisikia injili wakati wa Nuhu na kuokoka, ni watatu tu ndio walipona katika sodoma na gomora.

Je! hatuyajui haya? kwamba tunayatenda bila kujua? hapana, ni kwa makusudi kabisa na tunakimbilia kutoa sadaka kubwa kanisani ili Bwana apendezwe na sisi, tunajikita kufanya hili na hili kufanya dhehebu letu liwe kubwa, hilo dhehebu ni kitu gani mbele za Mungu? Biblia ndio KANISA na pumzi yake ni Roho mtakatifu
Au je! Sauli hakufanya jambo zuri kumletea Bwana kondoo walionona ili amtolee sadaka Bwana? lakini lilikuwa chukizo mbele za Bwana maana aliagizwa kampige amaleki na uue chochote bila kuchukua chochote. tuseme leo kujaa kwa dhehebu ni bora kuliko kuwafanya watu waache dhambi? inawafaidia nini maana ni bora wasingeokoka kabisa, ndivyo biblia inavyosema..,
15Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingikuwa heri kama ungekuwa baridi au moto 16Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu
Kama wewe umempokea kristo ishi kama kristo, na kama huwezi kuishi kama kristo basi achana naye. Maana hakuna utakachomtolea Bwana aondoe hiyo dhambi ya makusudi unayoifanya maana sehemu yako wewe(vuguvugu) na mtu asiyemwamini kristo ni moja nayo ni jehanamu.

Wapendwa nasema kweli, wataostahili kwenda mbinguni kupitia unyakuo ni wachache waliojikana kwa habari ya ulimwengu huu. Si kwamba wewe huwezi, hapana, Yesu yupo ambaye amesema lisilowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu linawezekana na leo Yule Mungu anafanya kazi kupitia ofisi ya Roho mtakatifu, Kweli kwa akili zako huwezi lakini ukitubu kwa kumaanisha kabisa, Roho mtakatifu atakupa uwezo wa kuacha na kuishinda dhambi. Tabia ambazo tunaziona katika muonekano wa nje ni dhahiri ndivyo ulivyo ndani, hukosi kuwa mwasherati kwa siri, mzinzi kwa siri, msengenyaji, mfiraji.
Unachopaswa kuangalia ni NENO linasemaje sio mchungaji anasemaje, ni kweli wachungaji wamepewa kuijua injili na tunapaswa kuwasikiliza lakini bila kusoma Biblia wewe kama wewe, utaishia kukubali kila najisi wanayoingiza kila kukicha ndani ya kundi. Mwisho wa siku wanakufanya mbaya kuliko wao wenyewe.

Yesu alisema yeyote anayetaka kunifuata ajikane mwenyewe kisha auchukue msalaba wake! kujikana ni lazima sio ombi ndio uupate ufalme wa mbinguni. Yapo mawazo ya kidunia ambayo kwa sasa hayaonekani kama ni dhambi, mfano, 90% au zaidi ya wafanyakazi serikalini na binafsi ni wezi; maana yangu ni hii, mtu ameajiliwa kama fundi labda wa mitambo, baada ya kuzoea kazi anakwepesha wateja wasifike kwenye kampuni na badala yake anakuwa anawahudumia yeye kama yeye na hela yote inaingia mfukoni kwake, yaani hilo wao hawaoni kuwa ni makosa tena(wanasema kujiongeza), ila cha ajabu wanaficha kampuni isijue, na ikijua kazi hana. Sasa, nikuambie tu kitu kimoja kwamba hata kama ungejenga makanisa dunia nzima kama sadaka, motoni utaenda kama ukifa na hiyo tabia hujaitubu, na mara nyingi tabia hii watu wengi hufa nayo maana hawaoni kama ni dhambi tena.

Tubuni! ukijua chochote kile ambacho si cha haki, kiache mara moja bila kujali kinakuingizia pesa kiasi gani. Kama ulinunua jina la mtu ukalisomea mpaka leo unalitumia katika kazi na mwenye nalo anaishi, katubu kwake na baadae kwa kampuni bila hivyo hautauona ufalme wa mbinguni. chochote kile kisicho halali ama haki kiache kabisa; huo ndio msalaba wako ambao unapaswa uubebe na kumfuata kristo. AU UTATOA NINI BADALA YA NAFSI YAKO?, Mungu hapokei hongo kwamba utampa hizo hela uupate ufalme wa mbinguni badala ya kwenda kuzimu.

shalom!

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

NAO WANIABUDU BURE!

NIMEWAPELEKEA TAUNI KAMA YA MISRI (CORONA) LAKINI HAMKUNIRUDIA MIMI