MADHARA YA KUTOKUWA NA KIU YA KUMJUA KRISTO

Nakusalimu katika jina la Yesu, mwokozi na Mungu wetu.Karibu tujifunze na ili tuzidi kukua katika kimo cha ujuzi na maarifa.

Unafahamu unavyoshikwa na kiu ya maji jinsi utakavyohangaika kuyapata, waswahili hadi wakasema maji ni uhai wakimaanisha umuhimu wake katika mwili ambapo husema 70% ya mwili ni maji. Mtu anaweza kwenda hadi wiki tatu bila chakula lakini ni siku tatu tu anweza kukaa bila maji. Kila mtu alishawahi kushikwa na kiu, kuna ile kiu inakushika halafu unakuwa mbali na maji kwa wakati huo; huwa inanyima raha kabisa. Ulishawahi kunywa soda kama mbadala wa maji?? kimsingi soda ni kimiminika kama maji isipokuwa ina kemikali yenye radha fulani ya utamu tofauti na ilivyo katika maji , ila cha ajabu soda huwa haindoi kiu, bali hutuliza dakika kadhaa kiu inarudi palepale, sijui kwa nini maana soda ni maji.

Hebu tuulete mfano wa kiu hiyo kiroho, mwili unahitaji maji kuzima kiu lakini mtu anao mwili na Roho. Kila roho imeumbiwa kiu ya ibada ama kuabudu, ndio maaana utakuta hata watu wasiomjua Mungu wana ibada zao. Wengine wanaabudu wanyama, wengine viumbe vya majini n.k. Kwa hiyo roho ina kiu ya kuabudu. Mtu anapozaliwa upya yaani kubatizwa baada ya kumpokea kristo hujazwa na Roho mtakatifu(Roho wa Yesu) na ujazo ule huanza chini kama tu unavyojaza maji kwenye chombo lakini ile kiu ya kumjua kristo huwa ni kubwa. Huwa anatamani kujua Zaidi na Zaidi yaani kukua na kuzidi kujaa Roho mtakatifu. Kujaa Roho mtakatifu si kunena kwa lugha bali kujaa maarifa ya mbinguni kupitia ufunuo katika maandiko matakatifu. Kunena kwa lugha ni ishara. tofautisha kunena kwa lugha kulivyo leo, huko kunaitwa kujinenesha kwa Lugha maana wananena kwa akili wala si kwa kujaa Roho.

Roho mtakatifu huchochea hii kiu kutaka kumjua kristo zaidi na zaidi hadi kuufikilia ukamilifu kama wa kristo ambao amesema tukifikia kimo hicho hatutaonja mauti kabisa
51Amin, amin, nawaambia, mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele.
yohana 8:51
Sasa kama ilivyo kwa mtoto anapozaliwa hulelewa kwa ukaribu na mama, vile vile Mungu huwa karibu sana na mtu anayempokea lakini baadae huwa anasogea mbali ili akuache ujue kusimama bila kushikwa mkono. Kiu ya kutaka kujua Zaidi ndio inayokufanya ukue, na ukuaji ni kupitia mafundisho, kusoma maandiko matakatifu na kumwomba Roho mtakatifu ambaye hutufunulia. Katika ukuaji mtoto huanza maziwa na baadae chakula kigumu. Mtu anayeukulia wokovu utamjua kwa kiu yake, mda wote hutaka kujua hili na lile na kuhitaji ufunuo. lakini mtu asiye na kiu ya kumjua Zaidi Yesu ni sawa na kusema umefungua mlango kwa shetani(rohoni ni mfu).

Tutazame matokeo/madhara ya kutokuwa na kiu ya kumjua kristo.
1.Kuiga namna/mitindo ya ulimwengu;
Ukianza kukosa kiu ya kumtafta kristo, dunia inakuwa tayari imeanza kuchomoza mizizi ndani yako, Mungu alisema watu wanaangamia kwa kukosa maarifa, na maarifa yapo ya aina mbili tu kiroho; maarifa ya mbinguni na maarifa ya kuzimu. Kwa hiyo kama ukikosa maarifa ya mbinguni basi unakuwa na yale ya ibilisi ambayo ili kuyapata ni kuchukua yale ya mbinguni na kuyageuza. Biblia imesema,
Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake
1yohana 2:15.

Jiulize, ulianzaje kuvaa suruali wakati wewe ni mwanamke? ulianzaje kupaka wanja, ulianzaje kufuga kucha, ulianzaje kuvaa modo, ulianzaje kunyoa kiduku, kwa sababu ulipoingia kanisani hukukuta huo ustaarabu. mitindo yote ya ulimwengu imetokea kwenye makasino, kumbi za starehe, madanguro na kupata nguvu kwenye luninga, ilikuwaje basi badala ya nuru yako iangaze kwa mataifa bali unachukua giza lao na kulileta ndani ya kanisa? Hata limetanda mpaka madhabahuni kwa ajili yako? watu wayatendayo hayo wapo kanisani kama miti mikavu, haiitaji maji maana haina kiu. Katoliki ni dhehebu lililo na hawa watu maradufu, walokole pia siku hizi kasi yao ni ya hatari sambamba na madhehebu yote. Tazameni muone wenyewe, Mungu wanamjua mdomoni tu ila mioyo yao iko mbali. Sawa na kusema unamwita Yesu lakini mkononi umeshikilia sanamu, Unajua kitachotokea? kasome Ezekiel 14:1-10.

2.Kupoteza kiu kunakufanya Kuzoelea wokovu.
kama kiu hamna, kuhudhuria kanisani inakuwa kama desturi tu, uasherati wapendwa kwa wapendwa linakuwa jambo la kawaida kwako. Unajua ni makosa lakini unakaza shingo. yaani hapa utawakuta waimbaji wazuri lakini matendo yao ni kama walishurutishwa kumpokea Yesu. Mtu unakuta yupo yupo tu, ameshiba udunia lakini kanisa ibada hakosi. Kwa lugha ngumu udunia wake anauita kizazi kipya, Yote ni kwa sababu hawana kiu ya kumtafta Yeye awapaye maarifa ya kuzishinda nguvu za shetani. Mathayo 16:18

3.Kutafta miujiza
Miujiza haikupeleki mbinguni wala haikufanyi kuwa mtakatifu. Haipo katika vigezo vinavyotufanya twende mbinguni, sasa unatafta ya nini? Miujiza inakuja ili kumfanya asiyeamini asadiki zizihirishwapo nguvu za Mungu. Hii siyo kiu ya kumtafta Mungu, Una kiu ya maji lakini hutaki maji bali soda. Mtu wa namna hii hana maarifa na kiu ya kuyatafta haimo ndani yake amebaki kutega siko asikie nani anatenda muujiza apate kuona kutendewa mmoja. Na kama huna maarifa ya mbinguni utajuaje kama ni muujiza wa kweli ama kiini macho? Hili nalo ni ubatili mtupu.

4.Kuzoelea maziwa(mafundisho mepesi)
Miaka nenda rudi upo kwenye uokovu lakini maarifa ya mbinguni aliyochuma hayana tofauti na mtu aliyempokea kristo miezi mitatu iliyopita. Nikupe mfano mdogo wa mtu ambaye amenifundisha wakati naokoka katika darasa la waongofu, miezi michache iliyopita amefungua kanisa. siku moja tukiwa njiani kuelekea kanisa lake, nilimuuliza kuhusu majira tuliyopo sasa, akasema tupo miaka mitatu na nusu ile ya mwisho katika ile miaka saba ya mwisho ya unabii wa Daniel 9. halafu akasema ndio maana unaona wanasayansi wanasema kuna jiwe kubwa linakuja usawa wa dunia na likitua litaisambaratisha na huo ndio utakuwa mwisho wa dunia akatoa mfano wa sanamu ile aliyooneshwa Nebkadreza katika Daniel 2:31-35. lile jiwe lililoipiga ile sanamu lisilo kazi ya mikono ya mwanadamu na kuujaza ulimwengu, Yeye anasema ndio hilo jiwe linalotoka huko juu. Sasa, maana yangu hapo ni hii; Katika ile ndoto lile jiwe huwakilisha kristo na ile sanamu inawakilisha falme zote mpaka masihi anakuja na kuuharibu ulimwengu(mwisho wa dunia). kilichonishangaza ni haya maarifa yake ya kijiweni wala si fasili ya maandiko ama ufunuo. Nilimkatalia halafu nikamwambia fasili yake sahihi. Na haiishii hapo, lakini ninalotaka ujue katika mfano huu; nimemkuta kwenye uokovu, akanifundisha lakini leo anahitaji kujua kutoka kwangu; mwinjilisti aliyesomea maandiko na mimi sijawahi hata kukanyaga chuo chochote cha Biblia. Je nini kilichonitoa huko nyuma na kuja kumpita katika maarifa? kama si kiu yangu ya kumtafta Yesu? na maarifa hayo sikuyatolea kwa mchungsaji wala chuo cha Biblia. Nilirudi kwa mchungaji wetu, nikamwambia wazi juu ya maziwa anayowanyeshwa waumini na kumpa mifano dhahiri pamoja na huo. Hebu mtazame huyu huo mfano, Ukuaji wake huyu mtu umedumaa, mtu mzima anastahili chakula kigumu inakuaje unaridhika kushindia maziwa?

5.Kuwa kipofu kiroho.
Hapa ndipo mazagazaga mengi yalipo. Chukulia huo mfano juu, wale waumini wa huyu mtumishi wataufikia utimilifu? watajua majira ya kuijiliwa kwao? watakuwa na kiu ya kumtafta kristo kwa mda gani? wakikua watalishwa chakula kigumu ama maziwa? Na huyo mchungaji je? kazi ameacha ili kumtumikia Bwana, hao watu ishirini watampa fungu la kutosha family yake? si atataka kanisa liongezeke? atafanyaje liongezeke. Mungu anajibu maombi ukimwomba lakini hawezi kukupa kisichokustahili maana utaangamia kwa sababu huna maarifa.Kitakachofuata ni upofu, wale waumini hawatajua hata kama huyu mchungaji akianzisha miujiza ya uongo ili kuvuta watu, kwa sababu hawana maarifa na ujuzi wa kweli. watamnyenyekea mchungaji kuliko kristo, watamweshimisha hata akawa na jina. wengine pia kama wakatoliki wakaabudu sanamu na watakatifu wa zamani ambayo ni machukizo makuu, walimu wao na wao waumini washakuwa vipofu wote. ndio utakuta wanakuambia sisi ndio tuliandika biblia, sisi ndio kanisa la mitume na takataka nyingi kama hizo. Katika maandiko ulishawahi kuona upuuzi kama huo unaweza kumpeleka mtu mbinguni? kuna kitbu au mtume ama nabii katika Biblia anaitwa Katoliki? nabii anaweza kufanya uasherati na asitubu lakini akaokolewa kwa sababu ni nabii? Eli kuhani kilimtokea nini? Na Mwisho wake yote ni ubatili mtupu.

6.Kushindana na Mungu.
Baada ya upofu, kinachobaki wote wanaanza kushindana na Mungu, wanatukana watumishi wake, wanawaua wanabii wake, yaani hawataki kuhubiliwa Neno lingine Zaidi ya maziwa waliozoeshwa kwayo na chakula laini laini.
wawaambiao waonaji, Msione, na manabii, msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambineni maneno laini, hubilini maneno yadanganyayo
isaya 30:10

Waliowaua manabii katika israeli ni israel wenyewe; sio mataifa(wasiomjua Mungu). Waliomsulubisha Yesu ni kanisa(wayahudi) sio rumi, wanaotukana injili ni wakristo sio wapagani Hebu jiulize???
kama huutambui wakati wakujiliwa kwako, utalikana Neno la Bwana, wana wa israeli walimkana Yesu wapate kushika maagano yao, Yeremia alipigwa makofi hata na makuhani asitabili mabaya, Neno lilitimia na Yuda kutiwa nguvuni mwa babeli.
Leo mkatoliki atakuambia tuache na dhehebu letu, atakuambia Neno lawezaje kutoka kwako wewe unakaa kwenye vijikanisa vya uchochoroni, vibanda umiza, utuambie nini sisi na jengo letu kubwa na mali nyingi!

Mwisho kabisa, nikuambie kwamba tabia za mtu ama kanisa ama mchungaji ama mwamini asiye na kiu ni kuwa amemzimisha Roho mtakatifu ndani yake. Hapo ni kama saa isiyo na betri. Utatambuaje majira uliyopo? Ndugu wapendwa acheni udhehebu, mrudieni Bwana! Mkasome maandiko kwa usaidizi wake mtajua tumesimama kwenye ukingo wa nyakati. Acheni kutangatanga katika mawazo mawili, Amueni kumtumikia Mungu ama shetani. Sio vyote viwili(huku nusu na huku nusu), biblia mkononi na mavazi ya kahaba mwilini. Dhehebu langu zuri na kubwa na huyajui maarifa ya mbinguni.

Tubu leo, mtafte Mungu sio dhehebu, wala mchungaji wala padre, wala papa, wala maria mama wa yesu, wala petro, wala yohana. Ni Yesu pekee hakuna mwingine.
Tubuni ili msije mkaingia katika saa ya kuharibiwa iliyo karibu mno kuujia ulimwengu, hapo ambapo unyakuo utakuwa umeshapita.
Shalom!

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

NAO WANIABUDU BURE!

NIMEWAPELEKEA TAUNI KAMA YA MISRI (CORONA) LAKINI HAMKUNIRUDIA MIMI

JE! NAWEZA KUWA SAFI NAMI NINA MIZANI YA UDHALIMU!!